Historia ya mfuko

Mfuko wa Afya ya Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA Community Health Fund) ulianzishwa katika mwaka wa fedha 2006/2007 ukiwa na madhumuni ya  kuwahudumia wanajumuiya wa Chuo wakiwemo watumishi na wategemezi wao pamoja na wanafunzi waliokuwa wanasoma Chuoni ili kuboresha na kuimarisha afya zao.

Aidha, baada ya Serikali kuanzisha Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) na kuwa ni lazima kwa watumishi wote wa Serikali kujiunga nao na kwa mujibu wa kanuni za usajili, Mfuko wa Afya wa Jumuiya ya SUA (SCHS) ulibadilika na kuwa ni Mfuko wa hiari kwa wanaopenda kujiunga nao bila kuhusisha wanafunzi wa Chuo kwa vile na wao wanapewa nafasi ya kujiunga na Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF).

Hivyo, kuanzia Mwezi Juni 2017 ambapo Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo katika mkutano wake wa 147 uliofanyika tarehe 29 Juni 2017 liliridhia sheria na kanuni za Mfuko wa Afya wa Jumuiya ya SUA (SCHS) na kuwa skimu ya ziada (Supplementary Scheme) katika kutoa huduma za afya kwa maana kwamba unaanza kutumika kumgharamia mwanachama na mnufaika wa Mfuko huo katika huduma za afya na matibabu baada ya huduma za NHIF na Mifuko mingine kuf ika ukomo.

Mfuko huu unagharamia huduma za afya na matibabu zinazotolewa katika Hospitali za Chuo, Hospitali za Serikali na baadhi ya Hospitali binafsi zilizopo ndani ya nchi, maduka binafsi ya madawa ya binadamu na kuchangia gharama za usafiri wa kawaida wa jamii mgonjwa anapopata rufaa kwenda kutibiwa katika hospitali zilizopo nchini na baadhi ya gharama za matibabu ya nje ya nchi.